Sunday, June 13, 2021

KILA MTU NA AMHESABU MWENZIWE KUWA BORA KULIKO NAFSI YAKE

 KILA MTU NA AMHESABU MWENZIWE KUWA BORA KULIKO NAFSI YAKE



Wafilipi 2:3

_[3]Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, *kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake.*_



Kati ya vitu ambavyo vitaondoa migogoro katika maisha yetu, huduma, familia na ndoa zetu basi ni ile hali ya *_kumhesabu mwenzako kuwa bora kuliko wewe._*


_Neno la Mungu linasema kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake._


Maana yake usijione wewe ni bora kuliko wengine bali uwaone wengine ni bora kuliko wewe.


Leo hii kitu kinachosababisha mashindano kati ya mtu na mtu ni kwa sababu mmoja anajiona ni bora kuliko mwingine. Hiyo ndio imepelekea majivuno na kiburi. Kwa sababu, kujiona bora kuliko wengine hicho ni kiburi.


Mtu anayejiona bora kuliko wengine huwa ana dharau na hautamsikia akiwasifia au kuwapongeza wengine ila anataka yeye asifiwe.


Mtu anayejiona bora kuliko wengine huwa ana tabia ya kupinga, kukosoa na kuhukumu wengine.


Mpendwa kama unataka umuone Kristo katika maisha yako, familia/ndoa au huduma yako basi jifunze kuwaona wengine ni bora kuliko wewe.


Ukiwaona wengine ni bora kuliko wewe utakuwa tayari kuwasikiliza na kujifunza kutoka kwao.


Ni muhimu ufahamu kuwa haujui kila kitu na hauwezi kufanya kila kitu na hauna kila kitu. Vipo vitu vingi sana ambavyo hauna na wapo watu wanavyo.


Ukiweza kumuona mwenzako ni bora kuliko wewe ndipo utanufaika na kitu Mungu alichoweka ndani yake kwa ajili yako ambacho wewe hauna.


Siku ya leo mwombe Mungu akupe neema ya kuwahesabu wengine ni bora kuliko wewe. Hata kama wamewahi kukosea lakini endelea kuwahesabu kuwa wao ni bora kuliko wewe.


Muone mzazi wako ni bora kuliko wewe, muone pia mtoto wako ni bora kuliko wewe. Muone mke/mume wako ni bora kuliko wewe. 


Muone kaka yako, dada yako au rafiki yako ni bora kuliko wewe. Muone mchungaji wako ni bora kuliko wewe, muone mshirika wako ni bora kuliko wewe.


Ukimuona mwenzako ni bora kuliko wewe utaweza kumpenda, kumsamehe, kumvumilia na kushirikiana naye na kumsaidia.



 ```WEWE NI BORA KULIKO MIMI``` 




*B Malachi*

No comments:

Post a Comment